Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu imefunguka na kudai kurejea kwa Mbunge huyo kwa sasa itachukua muda mrefu zaidi tofauti na awali ilivyokuwa kutokana na upasuaji aliyoufanya siku mbili hizi zilizopita.
Hayo yamebainishwa na msemaji wa familia Alute Mughwai ambaye pia ni Kaka wa Lissu baada ya kumalizika salama oparesheni wa mguu wake nchini Ubelgiji ambayo inakuwa ya 19 tokea alipoanza kufanyiwa matibabu tangu alipopatwa na matatizo.
"Miezi sita imepita hatusikii lolote kabisa kuhusiana na aliyehusika na tukio la kupigwa risasi Tundu Lissu au lile gari lililotumika kufanya uhalifu limepatikana au namna gani? wala bunduki iliyotumika kufyatua zile risasi hatujapata maelezo yeyote. Hakuna hata senti moja iliyotolewa na Bunge kwaajili ya gharama za matibabu za Mhe. Mbunge wao Lissu", amesema Mughwai.
Pamoja na hayo, Alute ameendelea kwa kusema "limejitokeza tatizo jingine sasa hivi kwamba anahitaji kufanyiwa upasuaji mwingine mdogo ili kuweza kuipanga mifupa yake vizuri maana yake ni kwamba muda utaenda kidogo mpaka kurudi kwake nchini Tanzania".
Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 7, 2017 na watu wasiojulikana akiwa mjini Dodoma na kisha baadae kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu ambapo huko alifanyiwa oparesheni kadhaa katika mwili wake na mwishowe kupelekwa nchini Beljium kwa matibabu zaidi ambapo Machi 14, 2018 amefanikiwa kufanyiwa oparesheni ya 19.
No comments: